Subscribe:

Ads 468x60px

Labels

Shambulio la Dar es Salaam:Maswali muhimu ambayo hayajajibiwa kuhusu shambulio la bunduki

t

CHANZO CHA PICHA,REUTERS

Siku ya jana, jiji la Dar es Salaama, Tanzania lilisimama kwa muda kufuatia mtu mmoja kufanya mashambulizi ya risasi na kusababisha vifo vya watu wanne; askari polisi watatu na mlinzi mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi ya SGA.

Baadaye mtu huyo aliuawa na Polisi, mbele ya geti la ubalozi wa Ufaransa nchini humo, katika barabara ya Al Hassan Mwinyi, baada ya majibizano ya risasi yaliyodumu kwa dakika kadhaa.

Kwa Mujibu wa Mkuu wa operesheni za polisi, Liberatus Sabas, akitoa taarifa za awali alisema mbali na vifo hivyo pia watu sita walijeruhiwa.

Tangu kutokea kwa tukio hilo, kumekuwa na taarifa nyingi zikisambaa mtandaoni kuhusu tukio hili na maswali mengi yakiibuka, lakini kati ya hayo maswali haya manne yanaendelea kusubiri majibu

1: Mshambuliaji huyu ni nani?

Licha ya kusambaa kwa jina na picha za mtu anayedaiwa kuhusika na tukio hilo, Jeshi la polisi halijajitokeza mpaka sasa kumtaja ni nani hasa.

  • Je ni raia wa Tanzania ama kutoka nje ya Tanzania? anajishughulisha na nini hasa?

Duru pia zinaonesha kuwa askari polisi jjijini Dar es Salaam wameichukua familia ya mtu ambaye amekuwa akidaiwa kutekeleza shambulio hilo. Hata hivyo polisi nchini humo haijathibitisha iwapo familia hiyo imechukuliwa kwa ajili ya mahojiano ama kulinda usalama wao kutokana na kusambaa kwa picha za mtu huyo mitandaoni.

Hakuna mwenye uhakika wa asilimia 100 juu ya mshukiwa huyo, ingawa mashuhuda na wengine wanaojitokeza wanajaribu kuelezea haiba yake.

"Nilivyoenda baharini, tukakutana na yule mtu kavaa shati ya drafti ya mikono mifupi', anasema mama mmoja mbele ya vyombo vya habari vya Tanzania aliyedai kukutana na mtu huyo dakika chache kabla ya kuanza kushambulia."

"Tulivyokutana naye, yule mtoto mdogo kamsalimia, yule baba kapokea, ila Kiswahili chake sio cha huku (Tanzania)," aliongeza shuhuda huyo.

Mshambuliaji huyu anaongea Kiswahili ila kwa mujibu wa mama huyu Kiswahili chake hakijanyooka akimaanisha kama sio cha Tanzania. Swali hapa, Kiswahili chake sio cha Tanzania;

  • Je ni Kiswahili cha nchi gani?
  • Je inawezekana ametoka nchi nyingine zinazozungumza Kiswahili?
  • Je hakuna watanzania wenye kuzungumza Kiswahili kwa lafudhi isiyo ya lahaja ya kawaida?

2: Alipata wapi silaha?

Swali lingine linaloibuka hapa ni wapi mtu huyu alipata silaha za kufanya mashambulizi haya?

Taarifa za awali za polisi zinasema alipora bunduki mbili za askari aliowaua kwa bastola, lakini je bastola inayodaiwa kutumika kuwaua askari hao aliipata wapi?

  • Anaimiliki kihalali?
  • Ni mtu mwenye uwezo kifedha na mali kiasi cha kuhitaji kumiliki silaha?
  • Au ana maadui wengi?

Kumiliki silaha Tanzania inaruhusiwa kwa kufuata utaratibu, lakini wanaomiliki silaha wengi nchini humo ni watu wenye nafasi za juu kiungozi ama kimaisha.

  • Je mtu huyu alikuwa na sifa hizo?

Hakuna mwenye uhakika, Jeshi la Polisi litasema.

3: Alikuwa na dhamira gani hasa?

Hili ni swali muhimu ambalo majibu yake yanaweza kutoa picha ya hasa kwa nini mshambuliaji huyu aliamua kufanya mashambulizi yale na kusababisha vifo vya Polisi watatu na mlinzi mmoja, kabla na yeye kuuawa.

Inawezekana angekuwepo hai, angekuwa na majibu ya uhakika wa dhamira ya kufanya alichokifanya, lakini swali la alikuwa na dhamira gani? Mpaka sasa linasalia vichwani mwa watu.

Wakati umma wa watanzania ukisubiri taarifa rasmi za Jeshi la Polisi, labda kwa uchunguzi wao wanaweza kusema dhamira ni nini hasa, wapo wanaolitazama tukio hilo na kulihusisha na ugaidi na wengine kuhusisha na visasi. Hakuna ushahidi na uthibitisho wa hilo.

Lakini wapo wanaohoji kama tukio la kigaidi;

  • Kwa nini mtu huyu hakuonekana kuwalenga raia?
  • Licha ya kwamba alikuwa na nafasi, silaha na muda wa kutosha wa kufanya hivyo?
  • Kwanini hakuwashambulia raia?
  • Na kama ni kisasi, kwanini askari?
  • Ambao ni walinzi wa watu na mali kisheria?
  • Au aliwaona ni watu ambao wangeweza kumdhuru?

"Ni mapema sana kusema ni kwanini mtu huyu ameenda kufanya vile, uchunguzi utabaini," alisema Mkuu wa operesheni za polisi, Liberatus Sabas na kuthibitisha kwamba wameshaanza uchunguzi.

4: Kwanini mashambulizi katika eneo hilo?

Kwa mujibu wa taarifa za Polisi tukio hili limetokea katika makutano ya barabara ya Kenyatta na Kinondoni, alipoanza kuwashambulia askari na kuchukua bunduki zao zinazoonekana ni aina ya AK47, kabla ya kuelekea mbele ya ubalozi wa Ufaransa na kutumia kibanda cha nje ye geti la ubalozi huo kujificha akiendelea kushambuliana na Polisi. Amefia hatua chache kutoka kwenye geti la ubalozi huo.

Lakini eneo lilipotokea tukio hili, kwa mfano alipoanzia kuwafyatulia risasi Polisi na kuwaua ni pembeni ya makazi ya balozi wa Uingereza nchini Tanzania na pembeni ya barabara hiyo kuna ubalozi wa Urusi.

Eneo alipofia mshambuliaji huyo ni kwenye geti la ubalozi wa Ufaransa, eneo ambalo si mbali na makazi ya balozi wa Zambia, ubalozi wa Kenya na makao makuu ya benki ya KCB na Benki ya Stanbic.

Lakini pia si mbali sana na kilipo kituo cha Polisi cha Salender. Unaweza kujiuliza uthubutu gani alioupata mshambuliaji huyu, kiasi cha kwenda kufanya mashambulio hayo kwenye eneo la aina hii, ambalo kawaida ulinzi wake mkubwa haufanani na maeneo mengine?

  • Kuna mtu yuko nyumba yake?

Mbali na kusema ni mapema kusema dhamira ya mtu huyo kufanya mashambuli hayo nini, Mkuu wa operesheni za polisi, Liberatus Sabas alisema 'uchunguzi utabaini', na kuthibitisha kwamba Jeshi la Polisi limeshaanza kufanya uchunguzi wake.

0 comments:

Post a Comment

Asante kwa kusoma habari hii! Tafadhali acha tupia maoni yako HAPA!