Katika mitandao ya kijamii
kumesambazwa habari zikimnukuu msemaji wa CCM kutoa madai mbalimbali ya
uzushi katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu CHADEMA baada ya
CHADEMA kuendelea kutekeleza mikakati na mipango yake ya kuwaunganisha
watanzania kupitia falsafa ya ‘nguvu ya umma’ katika kuchangia vuguvugu
la mabadiliko (M4C) katika maeneo mbalimbali nchini.
Nitatoa tamko kamili na kueleza
hatua za ziada baada ya kupata taarifa iliyotolewa kwa ukamilifu, hata
hivyo kuhusu madai yaliyokwisha sambazwa kwenye mitandao ya kijamii na
CCM nachukua fursa hii kutoa kauli ya awali kama ifuatavyo: Kuibuka huku
kwa CCM na kufanya propaganda chafu ni ishara ya kwamba CCM inaumizwa
na namna ambavyo watanzania wanajitokeza kuunga mkono CHADEMA kwa hali
na mali hivyo CCM sasa inatapatapa kujaribu kudhibiti wimbi la
mabadiliko kwa kutumia siasa chafu.
Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya
Kikwete anapaswa kueleza watanzania iwapo mikakati hiyo michafu ina
baraka zake na za serikali anayoiongoza kwa kurejea pia madai
yaliyotolewa na Waziri wa Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Steven
Wassira kuwa CHADEMA itasambaratishwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa
mbinu mbalimbali. CCM kwa kuwa imekuwa na kawaida ya kufanya usanii
kuhalalisha fedha haramu kama ilivyofanya kwenye chaguzi zilizopita
baada ya viongozi waandamizi wa CCM na makada wake kuchota fedha za
chafu kifisadi kama zile za kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA)
na vyanzo vingine vichafu na kuzisafisha kupitia harambee za hadaa
zilizofanywa na CCM kwa nyakati mbalimbali; inataka kuichafua CHADEMA
inayopata fedha kutoka vyanzo halali kwa njia za wazi ili kukatisha
tamaa umma wa watanzania unaochangia vuguvugu la mabadiliko. Viongozi wa
CCM wameamua kujidanganya, kuidanganya Serikali yao na kujaribu
kuwapotosha watanzania lakini CHADEMA inatambua kwamba watu wachache
wanaweza kudanganyika kwa muda mchache lakini si watu wote wakati wote;
na kwamba watanzania wa leo kwa uwingi wao hawawezi kudanganyika na
uzushi wa kijinga wa CCM.Ni ukweli ulio wazi kwamba CHADEMA imekuwa
ikifanya harambee kwa uwazi kwa nyakati mbalimbali katika kumbi na
katika mikutano ya hadhara ikiwemo ya vijijini ambapo michango hutolewa
kwa uwazi, aidha michango kwa njia ya simu inaweza kufuatiliwa na
kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba watanzania wameamua kuchangia
mabadiliko ya kweli.Madai ya CCM kuwa CHADEMA imepokea au itapokea
mabilioni ya shilingi kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi na narudia kwa
mara nyingine tena kuitaka CCM itaje majina ya serikali, taasisi ama
makampuni ya nje ambayo CCM inadai kwamba CHADEMA imepokea mabilioni ya
shilingi katika siku za karibuni au inatarajia kupokea.
Badala ya CCM kuisingizia
CHADEMA ilipaswa CCM ieleze watanzania orodha ya vigogo wa Serikali
inayoongozwa na wanachama waandamizi wa CCM ambao wanaelezwa kuwa na
akaunti nchini Uswisi na nchi zingine wakituhumiwa kupewa fedha za
kifisadi kutoka kwa makampuni ya utafutaji wa mafuta, gesi asili pamoja
na uchimbaji wa madini.
CCM ilipaswa ieleze watanzania
sababu za kuendelea kusuasua kujivua magamba ya ufisadi kinyume na
maazimio ya CCM yaliyofikiwa baada ya msukumo wa CHADEMA kutaja orodha
ya mafisadi kwa kuwa kati ya mafisadi hao ni pamoja na viongozi wa CCM
walioiingiza nchi katika mikataba mibovu.
Ikumbukwe kwamba madai haya si
mapya kutolewa na CCM, yaliwahi kutolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa
Wanawake wa CCM (UWT) Sophia Simba mara baada ya uchaguzi mkuu wa 2010
akidai kuwa CHADEMA imepokea fedha kutoka mataifa ya ulaya kwa ajili ya
kufanya maandamano ya kuiondoa CCM madarakani.
Itakumbukwa kwamba wakati huo
nilimtaka ataje nchi hizo na kueleza kusudio la kumchukulia hatua zaidi
na kwa upande mwingine niliyataka mataifa hayo ya Ulaya yatoe kauli
kuhusu madai hayo. Izingatiwe kwamba mataifa hayo yalikanusha madai hayo
ya CCM na Sophia Simba mwenyewe alikana kuwa hakuna madai hayo dhidi ya
CHADEMA.
Nimeelezwa kuwa CCM imetoa
madai mengine ya uzushi kuwa CHADEMA inapewa mabilioni toka nje kwa kuwa
nchi imegundua rasilimali za mafuta na gesi na kudai kuwa fedha hizo ni
kwa ajili ya kuiweka nchi rehani. Madai haya yaliwahi kutolewa pia na
Katibu wa CCM wa Fedha na Uchumi Mwigulu Nchemba na nikamtaka Waziri wa
Mambo ya Nje Benard Membe kutaja nchi hizo na mikataba hiyo hata hivyo
mpaka sasa hakuna kiongozi yoyote wa CCM na Serikali aliyejitokeza
kutaja CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni kutoka nchi gani na kwa
mikataba gani.
CCM inatoa madai hayo kuhamisha
mjadala baada ya CHADEMA wa uongozi bora, sera makini, mikakati sahihi
na oganizesheni thabiti kuwa mstari wa mbele katika kutetea rasilimali
za taifa na watanzania kutambua kwamba taifa letu litaepushwa kutumbukia
kwenye laana ya rasilimali kwa kuiondoa CCM madarakani katika chaguzi
za mwaka 2014 na 2015 na kuichagua CHADEMA.CCM na Serikali yake ndiyo
imekuwa kinara wa kupokea fedha kutoka nje kwa kisingizio cha misaada na
kuingia mikataba mibovu na mataifa ya nje pamoja na makampuni ya kigeni
na kuachia mianya ya uporaji wa rasilimali za nchi na CHADEMA imeanika
hali hii kwenye orodha ya mafisadi kwa kutaja majina ya viongozi
waliohusika kwenye mikataba ya madini na tutaendelea kufanya hivyo hata
katika masuala ya mafuta na gesi ambayo tayari vigogo wa Serikali
inayoongozwa na CCM wameshaanza kuingia mikataba mibovu na kuingiziwa
fedha katika akaunti zao za nje ya nchi.
Hivyo, badala ya CCM kutoa
madai ya uzushi kuhusu CHADEMA kuingia mikataba na serikali au makampuni
ya nje, CCM ieleze watanzania imechukua hatua gani mpaka sasa juu ya
viongozi na wanachama wake waliongia mikataba mibovu kwenye rasilimali
muhimu nchini ikiwemo madini, mafuta, gesi na maliasili zingine za taifa
letu na kutoa mikataba hiyo hadharani ili watanzania waweze kuchukua
hatua za kufanya mabadiliko ya kweli.
Hivi karibuni Rais Kikwete
ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alisema kwamba serikali inayoongozwa na
CCM haitarudia makosa ya kuachia mianya ya ufisadi kwenye gesi; hivyo
CCM ilipaswa wakati huu kuwaomba radhi watanzania kwa ufisadi
uliofanyika kwenye madini na rasilimali nyingine na kuishukuru CHADEMA
kwa kuendelea kuwaunganisha watanzania wakati wote kusimamia mabadiliko
ya kweli.CCM badala ya kutishia kuwa ina mikataba inayoihusu CHADEMA
ingetoa mikataba hiyo na hali hii ya CCM inayoongoza Serikali kudai
CHADEMA kufanya mikakati, mipango na shughuli iliyo kinyume cha sheria
bila vyombo vya dola kuchukua hatua ni ishara ya CCM kukiri wazi kuwa
chama legelege chenye serikali legelege kimeshindwa kuongoza nchi na
badala yake kimejikita katika propaganda chafu.
CHADEMA tangu kuanzishwa kwake
imekuwa na makubaliano ya ushirikiano (MOU) bila masharti yoyote na
vyama rafiki vya ndani ya Afrika na duniani na makubaliano hayo yamekuwa
yakifikiwa kwa uwazi ikiwa ni sehemu ya CHADEMA kuwa na mtandao wa
kimataifa na hayajawahi kuhusisha wala hayatawahi kuhusisha CHADEMA
kusaidiwa mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kufanya kazi zake kama
inavyodaiwa na CCM. CHADEMA kimekuwa chama kiongozi kwa nyakati
mbalimbali kueleza viwango cha matumizi yake ya fedha na vyanzo vya
fedha husika huku kikitegemea kwa kiwango kikubwa michango ya wanachama
na wapenzi wa chama hapa nchini pamoja na kutumia kwa ufanisi ruzuku
inayotolewa kwa vyama vya siasa.
CCM imekuwa na kawaida ya kutoa
madai ya uzushi wakati mwingine yakiambatana na kutoa nyaraka za
kughushi inazodai kuwa ni za CHADEMA. Ikumbukwe kwamba wakati wa
uchaguzi wa mdogo wa Igunga, CCM ilitoa madai ya uzushi kuwa CHADEMA
inafadhiliwa na nchi za nje ikiwemo kupewa mafunzo ya ugaidi na kudai
kuwa tayari magaidi wameingizwa na CHADEMA toka nje katika uchaguzi huo;
hata hivyo katika mwenendo wa kesi ya uchaguzi ya Igunga Katibu Mkuu wa
CCM Wilson Mukama aliyetoa madai hayo alitoa ushahidi mahakamani kwamba
CHADEMA haijawahi kuleta magaidi bali kauli hizo za CCM zilikuwa ni za
siasa za uchaguzi. Hivi karibuni, CCM imeghushi waraka mwingine na
kuusambaza kile ilichodai kuwa ni maazimio ya kamati kuu ya CHADEMA ya
kupanga migomo ya walimu, madaktari na mipango mingine ya kuhujumu
serikali; hata hivyo waraka huo ulidhihirika wazi kuwa ni wa kughushi.
Mikakati yote hiyo michafu
hupangwa na CCM mara kwa mara wakati ambapo CHADEMA inaanza operesheni
Sangara na mikakati mingine ya kuleta mabadiliko nchini na kujipanga
kuiondoa CCM madarakani kama ilivyo sasa ambapo CHADEMA inaendelea na
operesheni katika mkoa wa Morogoro hivyo watanzania wanapaswa kuipuuza
CCM na kuendelea kujiunga CHADEMA na kuchangia mabadiliko kwa hali na
mali mpaka kieleweke.
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
12/08/2012- Dodoma
0 comments:
Post a Comment
Asante kwa kusoma habari hii! Tafadhali acha tupia maoni yako HAPA!