Baraza
la Sanaa la taifa, BASATA, limemfungia Shilole kutojihusisha na masuala ya
muziki ndani na nje ya Tanzania kwa mwaka mmoja.
BASATA limempa barua Shilole jana yenye
taarifa za kufungiwa kwake.
Adhabu hiyo imetolewa kufuatia tukio la
msanii huyo kupigwa picha za aibu wakati akitumbuiza nchini Ubelgiji miezi
kadhaa iliyopita.
Hii ni taarifa rasmi ya BASATA:
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kama msimamizi na
mratibu wa sekta ya Sanaa nchini limemfungia msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya
Zuena Mohamed kwa jina la kisanii Shilole kufanya shughuli za sanaa nchini kwa
muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe 24/07/2015 hadi tarehe 24/07/2016.
Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 09/05/2015
akiwa katika onyesho lake la Muziki nchini Ubelgiji alikiuka maadili ya kazi ya
sanaa mbele ya hadhira ya wapenda sanaa za Tanzania na hivyo akadhalilisha utu
wake na jamii ya Kitanzania kimaadili.
Pia itakumbukwa kwamba mnamo mwezi
Oktoba, 2013 BASATA ilimuonya na akakiri kwa kuomba msamaha kwa tabia yake ya
kucheza bila kuzingatia utu na maadili awapo jukwaani.
BASATA ilimpa nafasi ya kutoa maelezo
yake kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kitendo chake cha
kudhalilisha maadili, utu na sanaa ya Tanzania lakini akakaidi kutoa maelezo.
Hivyo basi BASATA imejiridhisha kwamba alikiuka maadili ya kazi ya sanaa kwenye
onesho lake la huko Ubelgiji makusudi na amekiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za
uendeshaji wa Sanaa.
Hivyo basi kutokana na ukiukwaji huo wa
sheria na kanuni za uendeshaji wa shughuli za sanaa nchini, Baraza la Sanaa la
Taifa chini ya Kanuni ya 30(1)(d) ya G.N 322 ya 2005 limemsimamisha
kujishughulisha na kazi za Sanaa nchini kwa muda wa Mwaka Mmoja tokea tarehe
24/07/2015.
Hivyo haruhusiwi kufanya au kushiriki
kwa namna yoyote ile shughuli yoyote ya onesho la sanaa nchini au nje ya nchi.
Iwapo atafanya kinyume cha hayo kutapelekea kupewa adhabu zaidi ikiwa ni pamoja
na yeyote yule utakaye shirikiana naye.
Ni matumaini ya Baraza la Sanaa la Taifa
kwamba wasanii na waandaaji wa shughuli za sanaa wataendelea kutambua umuhimu
wa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Shilole aliwahi kusema kuwa hata yeye
hakupenda kile kilichotokea jukwaani wakati akitumbuiza nchini humo kwa sababu
ilikuwa bahati mbaya na hakudhamiria kukaa uchi kama wengi wanavyosema.
Shishi ambaye ni mama wa watoto wawili
alisema kuwa nguo mpya aliyoivaa siku hiyo ndio ilimponza kwasababu hakuwa
ameifanyia majaribio ya kutumbuiza akiwa ameivaa.
“Kiukweli kwasababu hili jambo limetokea
inatakiwa nguo ninapoinunua niwe naifanyia training kwanza kabla ya kwenda
jukwaani, kwahiyo kwasababu ile nguo ilikuwa mpya kwangu na sikuweza kuijua
vizuri […] yaani hii nguo nimeikuta huku huku, nguo imekuja kunitokea bahati
mbaya wakati niko kwenye performance, ilitatuka wakati niko kwenye motion,”
Shishi aliiambia Clouds FM.
Aliongeza kuwa alisikitishwa na mtu
aliyempiga picha hizo na kuamua kuzisambaza mtandaoni bila kujua kuwa
itamuumiza yeye kama mwanamke.
“Nasisitiza tena sikudhamiria na wala
sikupenda hiyo kitu itokee, ila nasikitika kwamba kama mimi mwanamke yule mtu
aliyenipiga picha na kudhamiria kuziweka kwenye mitandao alikuwa na maana gani,
hakufikiria mimi nitaunmia kiasi gani au mashabiki wangu wataumia kiasi gani?
Ni mtu mbaya mwenye roho mbaya sijui nimuiteje huyo mtu aliyefanya hivyo, sio
mtu mzuri.”
Unachukuliaje adhabu hiyo? Ni halali ama
Shilole ameonewa?
Chanzo:Bongo5
0 comments:
Post a Comment
Asante kwa kusoma habari hii! Tafadhali acha tupia maoni yako HAPA!