Baada ya kuondolewa kwa vikosi vya kimataifa, Taliban ilienea Afghanistan, ikidhibiti karibu kila mji na jiji. Kwa nini Marekani ilikubali kuondoka baada ya miaka 20 ya mapigano?
Mnamo mwaka 2001, Nato iliifurusha Taliban kutoka Kabul baada ya mashambulio ya 9/11 huko New York na Washington.
Hata hivyo karibu miongo miwili baadaye, viongozi wa kundi la wanamgambo wa Kiislamu wamerudi katika mji mkuu wa Afghanistan, wakipiga picha za kujifurahisha katika ikulu ya rais na karibu nchi nzima ikiwa chini ya udhibiti wao.
Pengine kinachoshangaza zaidi ni kwamba haikuwa ushindi wa kijeshi wa Marekani na washirika wake wa Nato ambao ulisababisha mabadiliko haya, bali makubaliano ya amani yaliyojadiliwa kwa uangalifu.
Ni nini kilisababisha makubaliano hayo, yaliyosainiwa chini ya rais mmoja na kutekelezwa na mrithi wake, kwenda vibaya sana?
Kwanini Marekani iliweka makubaliano na Taliban?
Siku moja baada ya Minara Pacha kuanguka, wakati huo rais wa Marekani George W Bush aliahidi "vita hii itachukua muda na kutatua, lakini hatukosei kuhusu hilo, tutashinda". Kwa kweli, Marekani haikukaribia kupata ushindi wa kijeshi dhidi ya Taliban.
Ingawa kundi hilo, ambalo lilikuwa na wapiganaji wa al-Qaeda waliohusika na mashambulio ya 9/11, lilisukumwa nje haraka ya miji na Nato, ilitumia miaka kadhaa kujipanga tena na mnamo mwaka 2004 walikuwa katika nafasi ya kuanzisha uasi dhidi ya vikosi vya magharibi na serikali mpya ya Afghanistan.
Kwa kujibu kuongezeka kwa mashambulio, rais mpya wa Marekani, Barack Obama, aliongeza idadi kubwa ya wanajeshi mwaka 2009 na kufanya ongezeko la wanajeshi wa Nato nchini humo kufikia 140,000.
Hii ilisaidia kuwarudisha nyuma Taliban mara nyingine tena, lakini kwa athari ndogo ya muda mrefu.
Mgogoro ulipokuwa vita virefu kabisa vya Marekani, na kugharimu nchi kiasi cha dola bilioni 978 na gharama ya maisha ya watu 2,300, ilizidi kutopendwa na Wamarekani na wito wa kukoma kuhusika na vita hivyo ulikuwa mkubwa.
Wakati idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouawa kwa mwaka ilikuwa ndogo baada ya kuhamia rasmi katika jukumu la mafunzo na msaada mnamo 2014, Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani alisema mnamo 2019 kwamba "zaidi ya wafanyakazi wa usalama wa Afghanistan 45,000 wamejitoa sadaka kuu" katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Kukabiliwa na hali hii, mrithi wa Obama, Donald Trump, alianza kuzidisha mazungumzo na Taliban, akitia saini makubaliano mnamo Februari 2020.
Lilikuwa ni jambo ambalo alikuwa na furaha kuzungumza kuelekea uchaguzi wa urais wa mwaka huo.
"Kwa kweli, tumetoka Afghanistan, kama unavyojua,"aliiambia Axios news. "Tumekuwa huko kwa miaka 19. Tutatoka."
Makubaliano yalisema nini?
Marekani ilikubali kuondoa wanajeshi wake waliobaki kutoka Afghanistan na Taliban ilisema haitakubali al-Qaeda au kikundi kingine chochote chenye msimamo mkali kufanya operesheni zao katika maeneo wanayodhibiti.
Pia ilisema kwamba wafungwa 5,000 wa Taliban watabadilishwa kwa wafungwa 1,000 wa kikosi cha usalama cha Afghanistan na vikwazo vitaondolewa dhidi ya kundi la wapiganaji wa Kiisilamu.
Makubaliano hayo yalishirikisha tu Marekani na Taliban, na mpango huo ulikuwa kwamba Taliban itajadili na serikali ya Afghanistan baadaye ili kujua ni vipi na nani ataiongoza nchi hiyo baadaye.
Vikosi vya usalama vya Afghanistan - vilivyofundishwa kwa gharama ya dola za Marekani bilioni 88.32 na zaidi ya wanajeshi 300,000 kwa nadharia, walikuwepo kudumisha hali hiyo wakati mazungumzo yakifanyika.
Rais Trump - ambaye aliuelezea kama "mpango mzuri" kulingana na mshauri wake wa Usalama wa Kitaifa wa wakati huo John Bolton - alisema hadharani kwamba mpango huo ulikuwa na "nafasi ya kuwa mzuri sana".
Pande zote mbili zilizingatia makubaliano ?
Marekani kwanza ilianza kuondoa wanajeshi chini ya Trump. Mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Taliban na serikali ya Afghanistan yalianza mnamo Septemba, lakini suluhu haikuonekana kuwa karibu.
Licha ya ukosefu wa maendeleo, wapinzani wa Taliban walibaki wakishikilia kuwa mpango huo hautasababisha maafa.
"Hii sio Vietnam," rais wa Afghanistan aliiambia BBC mnamo Februari. "Hii sio serikali inayoanguka."
Mnamo mwezi Julai, msemaji wa Taliban alidai "ingawa tuna nguvu juu ya uwanja wa vita, tunazingatia mazungumzo ".
Labda inaelezea zaidi kwamba walikuwa wakichukua miji mikuu 10 kwa wiki wakati huo.
Rais wa sasa wa Marekani Joe Biden - ambaye licha ya kutokubaliana na Trump karibu katika kila sera - aliendelea kutekeleza makubaliano ya mtangulizi wake, akiwaambia waandishi wa habari mwezi uliopita "hatapeleka kizazi kingine cha Wamarekani kupigana huko Afghanistan bila matarajio mazuri ya kufikia matokeo tofauti ".
"Uwezekano kutakuwa na Wataliban wanaotawala kila kitu na kumiliki nchi nzima kuna uwezekano mkubwa," ameongeza.
Na licha ya matukio ya siku za hivi karibuni, inaonekana rais amekwama na uamuzi wake.
"Ikiwa kuna chochote, maendeleo ya wiki iliyopita yanasisitiza kwamba kumaliza ushiriki wa jeshi la Marekani nchini Afghanistan sasa ilikuwa uamuzi sahihi," alisema Jumatatu.
Lakini kwa wengi, maoni ya kiongozi wa Taliban Mohammad Abbas Stanikzai akiongea katika chumba cha hoteli ya kifahari baada ya kusaini makubaliano na jeshi lenye nguvu zaidi ulimwenguni mnamo Septemba mwaka jana itakuwa ya kweli zaidi.
"Hakuna shaka tumeshinda vita," alisema. "Hamna shaka."
Credit: BBC
0 comments:
Post a Comment
Asante kwa kusoma habari hii! Tafadhali acha tupia maoni yako HAPA!