Subscribe:

Ads 468x60px

Labels

MILA ZA KURITHIWA KWA WAJANE BADO ZIPO BONGO!..



Baada ya kumaliza msiba wa mume wangu, wanandugu wa familia yangu na upande wa marehemu mume wangu walikutana. Hiki kilikuwa kikao ambacho sitakisahau katika maisha yangu. Mengi nilisikia kabla, na hata marehemu mume wangu akiwa hai alijaribu kuniambia kuwa jamii zao zina utaratibu huo. Muda huo tulikuwa tukiongea kiutani, na hatukujua kuwa ipo siku mimi na yeye tutaachana.

‘Wanandugu wenzangu, msiba umeisha, ingawaje majonzi hayataisha kamwe, lakini tutafanyaje, muumba ndiye aliyetuumba, na ndiye anayetupa uhai, siku ikifika huna jinsi. Sisi tuliobakia ni marehemu watarajiwa, kwahiyo cha muhimu nikuombeana heri, na kuwaombea waliotangulia walale mahala pema peponi…’ Huyu alikuwa msemaji mkuu wa familia.

Mzee huyu nilimuogopa sana, huwa alikuwa akitutembelea mara kwa mara, na akiona tunaishi kinyume na taratibu za familia zao, anakuja juu na kukemea, alikuwa hataki utani, hata marehemu mume wangu alikuwa akimheshimu sana. Mzee wa mila na desturi!

‘Taratibu za kifamilia zipo pale pale, hatuna jinsi ya kuzikwepa, na mtu anapofariki tunajua nini kifanyike. Labda kwa kuelezea zaidi ni kuwa marehemu kaacha mke na watoto. Mali kwetu sio muhimu sana, kwani tunajua kuwa mali ni mali za familia yote, ndio maana tunashirikiana kifamilia.

‘Lakini tujue kuwa mali zinatakiwa kutunzwa, na mitihani kama hii ikitokea mali zinaweza kufujwa na hata kutoka nje ya familia, na hili kwetu miaka nenda rudi tumekuwa tukililinda. Watoto watakosa matunzo bora yanayoendana na mila na desturi zetu, lazima tuwe makini kwa hili. Na kwa hiyo basi, ili mali, mke na watoto wasipotee, wasitoke nje ya familia yetu , tumekuwa na taratibi nzuri kabisa. Taratibu ya kuhakikisha kuwa mjane anakuwa mikononi mwetu, na watoto wanaendelea kuwa na baba ndani ya familia….’ Akatulia na kuniangalia.

‘Kwahiyo mwana wetu mpendwa, usiwe na wasiwasi kabisa, maisha yako yataendelea vyema, na hutapata taabu kabisa, mali , watoto na wewe mtakuwa salama kabisa. Labda nikuulize, mliwahi kuongea lolote wewe na mume wako, kuwa ikitokea kitu kama hichi, wewe utapenda kuwa katika ulinzi wa nani …’ akanikaia macho

‘Ulinzi wa nani, baba naomba ufafanuzi kidogo, kwani ulinzi mkuu ni kumtegemea mungu, na sidhani kuwa ninahitaji mtu , kwani niliyemtegemea zaidi kaondoka, na sidhani kama nahitaji mtu mwingine katika umri wangu huu, mimi na watoto wangu inatosha…’ nikasema kwa majonzi na kuanza kulia.

‘Sawa tumekuelewa, na hilo tunalijua kwa mtu yoyote, inatokea hivyo kwa muda, lakini binadamu, tumepewa kitu Fulani, kusahau, na ni swala la muda tu utasahau kabisa, itafika siku, hutamkumbuka kabisa marehemu…hii lipo, na sisi kama wanafamilia tuna uchungu mkubwa zaidi sana, kwanii huyo aliyeondoka ni mwanetu, hatuwezi kupata mtoto kama yeye, labda mwingine kwa namna nyingine, lakini sio kama yeye. Wewe kama mke utakutana na jamaa ukampenda, na hata zaidi ya ulivyopendana na marehemu, hii lipo, na ni ubinadamu..’ akaniangalia kwa makini.

‘Sisi katika familia yetu tuna utaratibu, kuwa mke akifiwa, anakuwa chini ya ulinzi wa ndugu wa marehemu, kwa jina jingine unarithiwa. Hili wanalipinga sana watu wengi, lakini sisi tumelitekeleza vizuri miaka nenda rudi na limeleta manufaa makubwa, ndio maana unaiona familia hii ni tajiri, kwani utajiri wetu hautoki nje. Sasa wewe uliolewa ndani ya familia hii, na ukakubali yote, na hili huna budi ulikubali. Unawaona wanaume wote hawa, waliokaa mbele yako, wengine wana wake wengine hawana wake, unachotakiwa ni kumchagua mmoja wao na muongee naye, na akikubali basi utakuwa mke halali wa huyo ndugu, ama uwe mke wa pili kwake, au watatu au wa kwanza,…hilo halina mjadala mrefu…’

Nilishikwa na kigugumizi. Sikuamini masikio yangu, nilitamanai mume wangu arudi nimuambie kuwa mbona haya hukunielewesha zaidi, mimi nilidhani ulikuwa utani. Nililia, na kulia, lakini hakuna aliyenionea Huruma, wao walikazania utamaduni wao huohuo ndani ya familia yao.

Mimi ni mwalimu, na kuelimisha ni jadi yangu, nilijaribu kuwaelimisha ubaya wa hili jambo, lakini nilikuwa kama mtoto anayemfundisha mzazi wake kupika, wakati yeye kila siku anapikiwa na mzazi wake huyo.

‘Uamuzi ni ndio huo, mawili, ukubaliane kukubali haya, au kama hutaki, basi umaikana familia na hatuna jinsi, tutakupa kilicho chako, na kutuachia watoto wetu, ambao wana haki zaidi katika mali zetu…narudia tena, mali zetu, kwani mali zote unazoona hapa zimetokana na ushirikiano wa familia, wewe mwenyewe umeliona hili….’ Aliendelea kuelezea mengi, lakini akili yangu haikuwepo tena ndani ya kikao hicho.

0 comments:

Post a Comment

Asante kwa kusoma habari hii! Tafadhali acha tupia maoni yako HAPA!