Watoto hawa hawajui leo au kesho watakula nini, hakuna anayehangaika kuwatafutia chakula, wanapolala na njaa hakuna wa kumlilia na wakiumwa hakuna wa kumweleza hivyo huendelea na maisha yao hadi wanapopata nafuu au kupona kabisa.
Ukweli ni kwamba, watoto hawa hujisikia wapweke kutokana na jamii kubwa kuwakataa na kuwaweka katika fungu tofauti.
Kitanda chao ni barabarani na wengine mitaroni, baridi yote ya usiku na jua la mchana ni lao, hawajui kubadilisha nguo, zile walizovaa wiki iliyopita hadi leo hazijatoka mwilini.
Tumezoe kuwaona watoto wenye wazazi wakitoka nyumbani asubuhi na kurudi majumbani mwao jioni. Watoto yatima na waishio katika mazingira hatarishi hawana pa kwenda, popote wanalala.
Jamii imesahau kuwa watoto hawa ni sawa na wao, wanasikia njaa, baridi na maumivu sawa na wenzao lakini nani anashughulika nao?
Sisi tunasema kuwa, watoto hawa hawakuchagua kuwa yatima na kuishi mitaani, hawakuchagua kufiwa na wazazi wao, wamejikuta wapo mitaani na hawana la kufanya kama watoto wetu walivyojikuta wakiwa mikononi mwetu na wanapata kila kitu.
Waswahili wanasema, kinga ni bora kuliko tiba. Mashirika yasiyo ya kiserikali NGOs na yale ya kimataifa kama UNICEF na Serikali, wanashughulikia tatizo la watoto hawa wakiwa tayari mitaani.
Jambo la msingi, nguvu inayotumika kuwasaidia watoto hawa ingepaswa kuelekezwa kwenye kinga ili kutibu tatizo hilo kabisa. Sababu moja wapo inayochangia ongezeko la yatima na watoto waishio mazingira hatarishi ni migogoro isiyokwisha katika ndoa.
Umefika wakati wa Serikali kuratibu nguvu za NGOs kwa kuhakikisha mashirika hayo, jamii na wao wenyewe wanachukua hatua stahiki kuhakikisha tatizo hilo nchini linakwisha.
0 comments:
Post a Comment
Asante kwa kusoma habari hii! Tafadhali acha tupia maoni yako HAPA!